Mshirikishi wa Shirika la Msalaba mwekundu kaunti ya Kilifi, Kauthar Ali amesema kuwa mila na desturi za kimijikenda zimekuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya dhulma za kijinsia.
Akizungumza na CocoFm, Kauthar amesema kuwa wahasiriwa wengi wa dhulma za kijinsia wanakosa haki kutokana na suala la kulinda mila na desturi.
Kauthar ameeleza kuwa visa vingi vya dhulma za kingono vinahusisha watu wa karibu wa waathiriwa wa dhulma hizo huku waathiriwa hao wakiishia kukosa haki.
Aidha Kauthar amekemea hulka ya wanajamii kutatua kesi za dhulma za kijinsia kinyumbani akisisitiza haja ya kesi hizo kuwasilishwa Mahakamani.
Mshirikishi huyo wa Msalaba Mwekundu eneo la Kilifi amesema kuwa idadi kubwa ya wakaazi wa Pwani hawana ufahamu kuhusu haki zao hali inayopelekea wao kuendelea kufinyiliwa zaidi katika masuala mbalimbali.
Kauthar amekariri haja ya wananchi kuendelea kupewa hamasa za mara kwa mara kuhusiana na haki zao kwenye masuala mbalimbali ikijumuisha, afya na uongozi.
Amehoji kuwa ukosefu wa Mahakama tamba katika maeneo ya mashinani unapelekea wakaazi wa maeneo hayo kuendelea kukosa haki kwani wengi wao wanashindwa kufika Malindi au Kilifi ili kufuatilia kesi mbalimbali.
Taarifa ya Hamis Kombe
