Mifumo ya usimamizi wa SHA yapingwa Mahakamani

Mifumo ya usimamizi wa SHA yapingwa Mahakamani

Ombi la kikatiba limewasilishwa katika Mahakama Kuu ya Kiambu kupinga uhalali wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), mifumo ya afya ya kidijitali na mipango ya matibabu kwa maafisa wa umma.

Mlalamishi anadai kuwa mifumo hiyo ya ufadhili wa huduma za afya inaendeshwa nje ya sheria.

Ombi hilo lililowasilishwa na Francis Awino linazitaja taasisi na maafisa mbalimbali wa serikali, wakiwemo Wizara ya Afya, hazina ya taifa, mamlaka ya afya ya jamii (SHA), mamlaka ya afya ya kidijitali, tume ya utumishi wa umma na tume ya huduma kwa walimu, miongoni mwa wengine, kama washtakiwa.

Kulingana na nyaraka za Mahakama, mlalamishi anasema kuwa mipango hiyo ya ufadhili wa huduma za afya inayopingwa, inahusisha majukumu yanayohusiana na bima kama vile makato ya ada za bima, pamoja na uchakataji wa madai na usimamizi wa mafao bila idhini wazi ya kisheria.

Jaji Bahati Mwamuye amemuelekeza mlalamishi kuwahudumia washtakiwa wote kufikia Mei 8, 2026, huku majibu kwa ombi hilo na maombi yanayohusiana yakitarajiwa kuwasilishwa Mahakamani kufikia Mei 22, 2026.

Kesi hiyo itaendelea katika Mahakama hiyo.

Taarifa ya Joseph Jira