Afrika Forward Summit inahitaji trilioni 11 kufadhili Kilimo Afrika

Afrika Forward Summit inahitaji trilioni 11 kufadhili Kilimo Afrika

Licha ya Afrika kuwa na takribani asilimia 60 ya ardhi isiyotumika kwa shughuli za Kilimo bado inakabiliwa na pengo kubwa la ufadhili wa Kilimo kwa zaidi ya shilingi trilioni 11 kila mwaka.

Wataalam wanasema hali hiyo inadidimiza uzalishaji wa chakula, ukuaji wa biashara za Kilimo na uundaji wa ajira.

Swala hilo limesababisha viongozi wa Afrika, taasisi za kifedha pamoja na wadau mbalimbali wa kimataifa kuweka azimio jipya la kuimarisha ufadhili wa Kilimo barani Afrika.

Hata hivyo utiaji wa saini wa suala hilo itakuwa ni kilele cha Kongamano la Afrika Forward Summit inalofanyika jijini Nairobi na ambalo linafadhiliwa na serikali ya Kenya na Ufaransa.

Kongamano hilo linatarajiwa kutamatika leo, tarehe 12 Mei 2026 huku masuala mbalimbali muhimu ikiwemo uboreshaji wa kimaendeleo, uwekezaji wa kikanda na ukuaji wa kiuchumi yakiangaziwa.

Kongamano la Afrika Forward Summit inafanyika jijini Nairobi na kuhudhuriwa na marais 30 kutoka mataifa ya bara la Afrika

Wanaharakati zaidi ya 100 waliohudhuria Kongamano hilo waliwasilisha mapendekezo yao kwa viongozi hao wa Afrika, wakitaka kulindwa kwa raslimali za Afrika ikiwemo Madini, kupanuliwa kwa uhuru wa kibiashara kati ya mataifa ya Afrika na kuboreshwa kwa mifumo ya utawala na demokrasia.

Tayari Kenya na Ufaransa zimetia saini makubaliano ya kuanzisha ubia wa usafirishaji na maendeleo ya miundombinu ya bandari inayokadiriwa kuwa takriban shilingi bilioni 104.

Makubaliano mengine yanahusu uzalishaji endelevu wa mafuta ya ndege, na ushirikiano wa uchumi wa majini.

Nchi hizo mbili zilikubaliana pia kukuza mauzo ya majani Chai maalum ya Kenya kwa masoko ya Ufaransa na kuimarisha ushirikiano katika huduma za afya, elimu na mafunzo ya kiufundi.