Idadi kubwa ya familia zilizokuwa zikiishi karibu na Mto Tana katika kaunti ya Tana river zimeanza kuhama ili kutafuta maeneo salama ya kuishi kufuatia athari za mafuriko.
Familia hizo zimesema tayari mto huo umeanza kuvunja kingo zake kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, na kuathiri familia hizo.
Familia hizo kutoka vijiji vya Ziwani na Bula Punde katika eneo bunge la Garissa mjini, zimesema hazina mahali pa kuishi na watoto wao licha ya kuitikia wito wa Serikali na Idara ya utabiri wa hali ya hewa kuhamia maeneo salama.
“Tumeambiwa tuhame tuenda maeneo mengine salama kuepuka majanga lakini hatuna mahali pa kuenda, tumeondoka kweli katika makaazi yetu kwa sababu kumejaa marufiko baada ya Mto Tana kuvunja kingo zake hata hatuna mahali pakuishi watoto wananyeshwe, serikali ingetusaidia”, alisema mkaazi.

Athari za mafuriko katika vijiji vya kaunti ya Tanariver
Kwa upande wake, Gavana wa Tanariver Dhadho Godhana alisema japo serikali ya kaunti hiyo haijapokea idadi kamili ya walioathirika, juhudi zaidi zinaendelezwa kuhakikisha waathiriwa wanapata msaada huku akiwahimiza kuhamia maeneo salama.
“Tunashirikiana na baraza la magavana kuangalia vile tutasaidia watu wetu kupata msaada wa chakula na hata mavazi kwa sasa vijiji vingi vimeharibiwa na mafuriko lakini tunafatilia ili tujue ni watu wangapi wameathirika”,alisema Godhana.
Hata hivyo Kamishna wa kaunti hiyo Joseph Mwangi aliwarai wakaazi walio katika athari ya kuathirika na mafuriko kuchukua tahadhari na kuhamia maeneo salama, akisema serikali inalishuhulikia suala hilo.
Hata hivyo familia zilizoathirika zimeiomba serikali kuwasaidia na chakula cha msaada kwani sasa hali imekuwa ngumu kwao huku wakipendekeza serikali kuchimba mabwawa ili kuzuia mafuriko baada ya mto Tana kuvunja kingo zake.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
