Wakfu wa George Kithi unaoimarisha jamii kupitia kufadhili wa masomo ya wanafunzi werevu wanaokabiliwa na changamoto za ukosefu wa karo, misaada ya matibabu kwa wagonjwa kutoka Familia maskini pamoja na miradi ya kijamii, uliandaa hafla maalumu ya kutoa misaada ya masomo kwa kipindi cha masomo cha mhula wa pili.
Wazazi walionufaika na msaada huo walipokea stakabadhi za kuthibitisha misaada hiyo ya masomo.
Kwa mujibu wa Mratibu mkuu wa mipango ya Wakfu huo Mwanyule Baya Mweri, Wakfu huo unashughulikia miradi mingi ya kusaidia jamii.

Maafisa wa Wakfu wa George Kithi wamkabidhi mzazi hundi ya karo ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi werevu
Miongoni mwa miradi hiyo ni gari la kusafirisha miili kwa wale wanaokumbwa na changamoto za mazishi.
Wakfu huo pia unashughulikia msaada wa matibabu kwa wagonjwa wasiojiweza.
Wakati wa hafla hiyo wawaniaji nyadhifa mbalimbali za kisiasa ikiwa ni pamoja na ubunge, uwakilishi wa kina mama na Wawakilishi wadi wa Chama cha UDA waliendeleza kampeni zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali za kisiasa ikiwa ni pamoja na ubunge, Uwakilishi wa kina mama na Wawakilishi wadi wa Chama cha UDA wameelezea juhudi za kupiga jeki sekta ya elimu kaunti ya Kilifi
Aidha walikashfu vikali kisa cha unajisi na mauaji ya msichana wa miaka saba katika kijiji cha Kwa Nzai eneo la Mwezang’ombe katika eneo bunge la Kilifi kaskazini kaunti ya Kilifi.
Wazazi waliohudhuria hafla hiyo walichukua fomu za maombi kwa ajili ya usaidizi ujao wa masomo huku waliofadhiliwa wakiupongeza Wakfu huo.
Taarifa ya Lolani Kalu
