Mashirika mbali mbali ya kuangazia maslahi ya kijamii wameendelea kukongamana mjini Malindi katika kaunti ya Kilifi kujadili masuala ya haki na sheria miongoni mwa makundi tofauti katika jamii.
Katika siku ya Pili ya Kongamano hilo linaloongozwa na Shirika la Msalaba Mwekundu nchini, imebainika kuwa ukosefu wa hamasa kuhusu sheria miongoni mwa waraibu wa dawa za kulevya imekuwa changamoto miongoni mwao kujitetea wanapojikuta wameenda kinyume na sheria.
Abdhala Badlusi Mkurugenzi wa MEWA kitengo cha kusaidia waraibu hao, amesema hali hiyo imewaacha waraibu wengi kujikuta njia panda katika kupata haki.
Badhlus amesema sheria za nchi zinafaa kuangazia namna jamii hizo zitaweza kupata haki kama watu wengine, ili kuhakikisha kuna usawa katika jamii.
Vile vile suala la haki katika masuala ya afya limeangaziwa katika Kongamano hilo, wadau wakisema maafisa wa afya nyanjani wamekuwa na mchango mkubwa kuhamasisha jamii ya watu wanaoishi na virusi vinavosababisha ukimwi katika kufikia huduma za afya.

Mashirika mbali mbali ya kongamana mjini Malindi katika kaunti ya Kilifi kujadili masuala ya haki na sheria miongoni mwa makundi tofauti katika jamii.
Hata hivyo mawakili wa ngazi ya jamii maarufu Paralegals wanasema suala la unyanyapaa katika jamii limekuwa kikwazo kikubwa kwa makundi haya kuendelea na maisha ya kawaida, wakishinikiza jamii kuwakumbatia watu hao na kuwapa motisha.
Kauli za washikadau hao zimeunga mkono na Hakimu katika Mahakama ya Kilifi Ivy Wasike, akisema sheria inawajibisha kila mmoja kulinda haki za makundi ya wachache katika jamii ili kufikia huduma muhimu za kiserikali.
Hakimu Wasike vile vile ameitaka jamii kuhakikisha inawakubali walio katika makundi ya wachache, akisema changamoto za kimaisha zinazowakumba huenda ni kutokana na masuala mbali mbali ya kifamilia.
Kongamano hilo la Siku tatu linatarajiwa kukamilika Alhamisi hii.
Taarifa ya Joseph Jira
