Wakaazi waandamana kupinga mauaji ya mtoto Keziah Kilifi

Wakaazi waandamana kupinga mauaji ya mtoto Keziah Kilifi

Wakaazi pamoja na Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu katika Kaunti ya Kilifi wameandamana wakitaka idara ya usalama kuharakisha uchunguzi kuhusu mauaji ya kinyama ya mtoto wa miaka saba anayedaiwa kunajisiwa kabla ya kunyongwa, kisha mwili wake kutupwa karibu na nyumbani kwao katika kijiji cha Kwa Nzai, eneo la Mwezang’ombe.

Waandamanaji hao waliokuwa wamejaa huzuni na ghadhabu walitembea kutoka eneo la tukio hadi afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Kilifi wakitaka majibu kuhusu hatua iliyofikiwa katika uchunguzi huo pamoja na hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.

Wakaazi waandamana kushinikiza maafisa wa usalama kumtia nguvuni mshukiwa wa mauaji ya mtoto Keziah

Maafisa wa polisi wakiongozwa na Kamishna wa Kaunti Simon Mutisya waliwahakikishia wananchi kuwa mshukiwa mmoja tayari ametiwa mbaroni huku maafisa wa upelelezi kutoka idara ya DCI wakiendelea na uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wote waliohusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Maafisa hao pia waliwataka wananchi kudumisha utulivu na kuipa nafasi idara ya usalama kukamilisha uchunguzi, wakisisitiza kuwa haki itapatikana kwa familia ya mtoto huyo.

Hata hivyo, mkutano uliokuwa umepangwa kuwa wa amani na wa kutafuta suluhu uligeuka kwa muda baada ya baadhi ya vijana waliokuwa na hasira kuondoa hema lililokuwa limewekwa kwa ajili ya viongozi wa kisiasa kuwahutubia wananchi.

Taaridfa ya Elizabeth Mwende