Bwiwi la simanzi limeghubika wakaazi wa kijiji cha Kwa Nzai eneo la Mwezang’ombe kaunti ya Kilifi mapema leo baada ya msichana mwenye umri wa miaka 7 kupatikana amefariki baada ya kudaiwa kunajisiwa.
Wakaazi wa kijiji hicho wamekongama katika eneo la tukio kushuhudia maafisa wa usalama wakiuchukua mwili wa mtoto huyo aliyefanyiwa ukatili na mtu ambaye hajafahamika kwa sasa.
Kulingana na wazazi wa mtoto huyo Bernadict Keziah ambaye yuko gredi ya ya Pili, walimsaka usiku kucha katika sehemu mbali mbali bila mafanikio.
Familia hii inasema imeshtushwa na umati wa watu uliokuwa umekusanyika nje ya boma lao mapema asubuhi, wakati walipokuwa wanaendelea na juhudi za kumtafuta msichana wao.

Wakaazi wa Kwa Nzai eneo la Mwezang’ombe kaunti ya Kilifi wameghubikwa na wingu la majonzi baada ya mtoto wa miaka 7 kubakwa na kuuwawa
Babake msichana huyo Brandon Matuki pamoja na mamake Faith Namwezi wanasema walikuwa na matumaini makubwa na maisha ya mtoto huyo wa kipekee, waliyemtaja kama mpenda watu na mkakamavu masomoni wakitaka wahusika kutafutwa na kukabiliwa.
Baadhi ya majirani wa Karibu wa Familia hiyo wamekemea kitendo hicho cha kinyama, wakitaka viongozi bungeni kubuni sera za kukabiliana na wanaopatikana na hatia ya kutekeleza vitendo kama hivyo kwa watoto wadogo.
Mwili huo unahifadhiwa katika makafani ya Hospitali ya rufaa ya Kilifi mjini Kilifi, ukitarajiwa kufanyiwa upasuaji jumanne wiki hii huku maafisa wa polisi wakiendelea na uchunguzi wa mauaji hayo.
Taarifa ya Joseph Jira
