Visa vya mauaji ya Wazee kwa tuhma za uchawi vimetajwa kupungua kwa asilimia kubwa.
Mwenyekiti wa kituo cha Kaya Godoma Emmanuel Katana amesema eneo la Mrima wa Ndege eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi, limekuwa sehemu ya kuwahifadhi wazee kutokana na visa hivyo.
Katana amesema idadi hiyo imepungua kutokana na hamasa za mara kwa mara zinazoendelezwa katika jamii, pamoja na vijana kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuwaenzi wazee wao.
Alisema kuwa vijana pia wamejumuishwa kwenye hamasa hizo ili kuhamasisha vijana wenzao kuhusiana na athari ya kuwaua wazee kwa shutuma za uchawi, akisisitiza haja ya vijana kuwa mstari wa mbele kueleza wenzao kwani wazee wamekuwa kielezo chema kwa jamii.
“Tumefanya hamasa kwa jamii na hatua hiyo imetusaidia sana kudhibiti visa vya wazee wetu kupoteza maisha yao kutokana na shtuma za uchawi, na tutaendelea kuwaelimisha vijana”, alisema Katana.
Mwenyekiti huyo pia alisema jamii imemudu kumaliz unyanyapaa kwani idadi kubwa ya wazee wamerejea makwao licha ya wao kunusurika kifo hapo awali wakihusishwa na uchawi.
Taarifa ya Hamis Kombe
