Afisa wa usajili wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC eneo bunge la Kilifi Kaskazini kaunti ya Kilifi , John Mwawasi amesema wanapania kusajili wapiga kura wapya 13,316 katika zoezi hilo ambalo linakamilika leo Aprili 28 baada ya kuanza Machi 30.
Katika mazungumzo ya kipekee na Coco FM kwenye afisi za IEBC hapa mjini Kilifi, Mwawasi alisema kufikia Aprili 27 walikuwa wamefanikiwa kusajili wapiga kura wapya 12,999 na kwamba muda wa usajili hautaongezwa baada ya kukamilika leo.
“Itakuwa vyema kama wakenya watajitokeza kwa wingi kabla ya zoezi hili kukamilika kwani IEBC haitaongeza muda licha ya Viongozi na baadhi ya wananchi kupendekeza muda zaidi kuongezwa” alisema Mwawasi.
Mwawasi alisema vijana wengi walijitokeza katika zoezi hilo huku akitaja baadhi ya changamoto ambazo wamezipitia katika usajili wa wapiga kura wapya.
“Baadhi ya wananchi hasa vijana wanalalamikia ukosefu wa vitambulisho na wengine kutaka kulipwa ili kujisajili kuwa wapiga kura”Aliongeza Mwawasi
Mwawasi pia alisema usajili wa wapiga kura utaendelezwa katika afisi za IEBC na vituo vya Huduma Center.

Wakaazi wa Kilifi Kazkazini wakishiriki zoezi la usajili wa wapiga kura
Kwa upande wa wananchi ambao walifika katika afisi za IEBC Kilifi Kaskazini walieleza namna zoezi hilo lilikuwa huku wakitoa wito kwa wakenya wengine kujisajili kwa wingi kuwa wapiga kura ili washiriki uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2027.
Haya yanajiri huku Tume (IEBC) ikifanya kila juhudi kufikia azma yake ya kuwaandikisha wapiga kura wapya milioni 2.5 na kaunti za Nairobi na Kiambu zinaongoza kwa idadi ya juu ya wapiga kura wapya.
Kaunti za Lamu, Isiolo na Mandera zikiandikisha idadi ya chini ya waliojisajili.
Taarifa ya Janet Mumbi
