Baadhi ya wajumbe wa bunge la Seneti chini ya mpango wa Seneti mashinani wamefanya ziara katika majengo ya bunge la kaunti ya Kilifi na kupokelewa na Karani wa bunge hilo Michael Ngala.
Wajumbe hao wa sekta mbalimbali wa bunge la Seneti wakiongozwa na Daniel Chania, wametathmini masuala mbalimbali ya bunge la kaunti ya Kilifi kama lina uwezo wa kuandaa ziara ijayo ya Seneti mashinani.
Seneti Mashinani ilianzishwa chini ya kifungu cha 126 ibara ya kwanza ya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, kinachoruhusu kikao cha bunge lolote kufanyika mahali popote ndani ya taifa la Kenya na kuanza wakati wowote kitakapopangwa na bunge.
Malengo ya vikao hivyo katika kaunti ni pamoja na kuhamasisha umma kuhusu kazi za bunge na Seneti, kuimarisha ushiriki wa umma katika shughuli za Seneti kwenye ngazi ya kaunti sawa na kutoa hamasa kwa wananchi kwa lengo la kuhimiza ushiriki umma katika utawala.

Baadhi ya wajumbe wa bunge la Seneti chini ya mpango wa Seneti mashinani wamefanya ziara katika majengo ya bunge la kaunti ya Kilifi
Bunge la Seneti limeanza maandalizi ya vikao vitakavyofanyika nje ya Nairobi, ambavyo vinatarajiwa kufanyika mwezi Septemba 2026.
Kaunti ya Kilifi ni miongoni mwa kaunti zilizoteuliwa kuwa kati ya zile zitazoandaa vikao hivyo kwa ajali ya umma kuwa na uelewa zaidi kuhusu shughuli za bunge hilo.
Wajumbe hao walikuwa na malengo pia ya kubaini upatikanaji wa miundombinu na huduma muhimu ili kuiwezesha Seneti kufanya uamuzi.
Kaunti nyingine zilizowahi kuandaa Seneti Mashinani ni pamoja na kaunti ya Uasin Gishu mwaka 2018, ikifuatiwa na kaunti ya Kitui mwaka 2019, kaunti ya Turkana mwaka 2023 na kaunti ya Busia mwaka 2025.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
