Wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu katika eneo la Pwani wamefanya maandamano ya amani wakilalamikia hali mbovu ya barabara ya Mombasa-Malindi.
Wanaharakati hao wanasema ukarabati wa barabara hiyo hasa eneo la Mtwapa umechukua muda mrefu kukamilika na kuchangia kudorora kwa uchumi wa eneo la Pwani huku magari yanayotumia barabara hiyo yakiendelea kuharibika kila mara.
Wakiongozwa na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Vocal Africa Hussein Khalid, Wanaharakati hao walikosoa mwendo wa polepole wa ujenzi wa barabara hiyo, wakisema umegeuka kuwa tishio kwa usalama na shughuli za kiuchumi.
“Kila kukicha magari yanaharibika barabara ni mbovu, kwa hivyo tunaiambia serikali tunataka hii barabara iishe haraka iwezekanavyo”, alisema Khalid.

Wanaharakari wafunga barabara ya Mombasa -Malindi wakilalamikia ubovu wa barabara hiyo
Kwa upande wake, Khelef Khalifa wa shirika la MUHURI amekosoa jinsi miradi ya maendeleo katika eneo la Pwani inavyotekelezwa kwa mwendo wa kujikokota, akisema hali hiyo imelemaza utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
“Tukienda Feri, watu ambao wanavuka kwa feri ni laki nne kwa siku na magari elfu 20, hakuna daraja kila kitu kinatoka hapa kinafanywa huko kila kitu kinafanywa huko polisi wenyewe wanalalamika ni utovu wa usalama sasa tumeanza kupeleka barua wanaanza kujazajaza kwa mawe”, alisema Khelef
Wanaharakati hao sasa wanaitaka serikali kuharakisha ukamilishaji wa barabara hiyo ili kupunguza ajali, msongamano wa magari pamoja na kuboresha shughuli za biashara kati ya kaunti za Pwani
Taarifa ya Mwanahabari wetu
