Buriani Mama Dorothy Baya, 1947-2026

Buriani Mama Dorothy Baya, 1947-2026

Mwili wa Mama Dorothy Baya Mweri ambaye ni Mama mzazi wa bunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya umetolewa katika makafani ya hospitali ya rufaa ya Kilifi kaunti ya Kilifi.

Mwili wa Mama Dorothy umefanyiwa ibada fupi ya wafu nje ya makafani ya hospitali hiyo ikiongozwa na viongozi wa kidini kisha wananchi wakapata fursa ya kuutazama mwili ili kutoa heshima yao ya mwisho kwa marehemu.

Viongozi mbalimbali wa kisiasa pia walikuwa na nafasi ya kumpa mkono wa buriani Mama Dorothy wakiongozwa na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro na Mwenyekiti wa bodi ya hazina ya michezo na sanaa ambaye pia ni mgombea wa wadhfa wa useneta kaunti ya Kilifi Wakili George Kithi.

Viongozi wengine waliokuwepo kutoa heshima zao za mwisho kwa Marehemu ni pamoja Mbunge wa Ganze Kenneth Tungule, Mbunge wa Kaloleni Paul Katana, Mgombea wa wadhfa wa uwakilishi wa kike kaunti ya Kilifi Christine Zawadi, miongoni mwa wengine.

Msafara wa Marehemu baadaye ulielekea katika kijiji cha Dabaso eneo bunge la Kilifi Kazkani kaunti ya Kilifi kwa ibada ya misa ya wafu katika Kanisa la St Stephen Dabaso kabla ya halfa ya mazishi siku ya Jumatatu.

Marehemu amewaacha watoto 6, akiwemo Mbunge wa Kilifi Kazikazini ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa wengine bungeni Owen Baya, Askofu mkuu wa Kanisa la Kianglikana Dayosi ya Mombasa Alphonce Mwaro,Charity Mapenzi, Felix Mweri, Mercy Kadii na Catherine Harusi, pamoja na wajuu kadhaa.

Hata hivyo viongozi na wananchi wa tabaka mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria halfa ya mazishi ya Mama Dorothy itakayofanyika siku ya Jumatatu hapo kesho tarehe 6 mwezi Aprili mwaka huu katika kijiji cha Dabaso.

Mama Dorothy aliaga dunia tarehe 30 mwezi Machi, 2026.