EACC yarejesha mali ya shilingi milioni 281 zilizoporwa

EACC yarejesha mali ya shilingi milioni 281 zilizoporwa

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imefanikiwa kurejesha mali ya umma yenye thamani ya shilingi milioni 281 katika kaunti ya Mombasa.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Tume ya EACC ilisema mafanikio hayo yametokana na baadhi ya hukumu zilizotolewa Mahakamani na kuipa nguvu Tume hiyo kurejesha mali hizo zilizochukuliwa kinyume cha sheria.

Miongoni mwa mali zilizorejesha ni pamoja na vipande vya ardhi ambavyo viko kando ya barabara ya Shimanzi vyenye thamani ya shilingi milioni 175, ambayo ni mali ya Shirika la Reli nchini.

Vipande hivyo vya ardhi vinasemekana vilikuwa vimepeyanwa kwa watu binafsi kinyume cha sheria, lakini Mahakama ikabatilisha umiliki huo wa ardhi na kuamuru virejeshwe kwa Shirika la Reli nchini.

Hatua hiyo ilitokana na mzozo uliyokuwepo baina ya watu binafsi waliokuwa wakidai kwamba ni wamiliki halali wa ardhi hizo, huku Shirika la Reli nchini likishikilia kwamba ardhi hiyo ni yao na kuilazima Mahakama kuingilia kati.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi