Kiungo wa Arsenal, Eberechi Eze, aliiumiza tena Tottenham baada ya kufunga mabao mawili yaliyosaidia vinara hao wa Ligi Kuu ya England kuifunga Tottenham mabao 4-1 katika dabi ya kaskazini mwa London Jumapili.
Kikosi cha kocha Mikel Arteta kilimaliza msururu wa mechi mbili bila ushindi na kujitanua kileleni kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Manchester City walioko nafasi ya pili. Mbali na mabao ya Eze, mshambuliaji Viktor Gyokeres pia alifunga mabao mawili katika ushindi huo mkubwa.
Baada ya kukataa kujiunga na Tottenham msimu uliopita, Eze ameonekana kung’ara zaidi akiwa katika jezi ya Arsenal hasa dhidi ya wapinzani hao wa jadi. Gyokeres naye alituliza presha mapema kipindi cha pili, kabla Eze hajafunga bao la tatu na Gyokeres kukamilisha ushindi huo muhimu.
Kwa Gyokeres, aliyekuwa na msimu mgumu baada ya kuhamia kutoka Sporting Lisbon, mabao hayo yalikuwa ya ukombozi mkubwa, sawa na ilivyokuwa kwa Eze.
Arsenal walikuwa wameanza kuyumba katika mbio za ubingwa baada ya sare dhidi ya Brentford na Wolves, matokeo yaliyofufua matumaini ya Manchester City. Ushindi wa City wa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle ulikuwa umepunguza pengo hadi pointi mbili kabla ya dabi hiyo.
Kocha Arteta aliwahimiza wachezaji wake kuvumilia presha ya mbio za ubingwa, akisema yeyote asiyeweza kustahimili “kelele na mashambulizi” bora aondoke klabuni na kuwaachia wengine waandike historia yao wenyewe.
Hata hivyo, licha ya ushindi huo, hatma ya ubingwa bado iko mikononi mwa Manchester City. Iwapo kikosi cha Pep Guardiola kitashinda mechi zake zote 11 zilizosalia, kitachukua taji hilo bila kujali matokeo ya Arsenal katika mechi zao 10 zilizobaki.
Arsenal sasa hawajapoteza katika dabi nane zilizopita dhidi ya Tottenham. Mashabiki wao walifurahia ushindi huo huku wakikumbusha wapinzani wao kuwa hakuna uhakika wa kukutana tena msimu ujao.
Tottenham wako pointi nne tu juu ya eneo la kushuka daraja, huku wakiongeza idadi ya mechi bila ushindi hadi tisa katika mchezo wa kwanza wa kocha wa muda Igor Tudor baada ya Thomas Frank kutimuliwa.
Ingawa Tudor ana uhakika kwa asilimia mia moja kuwa klabu hiyo itasalia Ligi Kuu, hatari ya kushuka daraja bado ni tishio baada ya kushinda mechi mbili pekee katika 18 zilizopita.
Arsenal walitangulia kufunga dakika ya 32 baada ya Pape Sarr kupoteza mpira karibu na lango lao. Bukayo Saka alimchezea krosi Eze aliyepiga voli safi kutoka umbali wa yadi 10 na kufunga bao la kwanza.
Hata hivyo, uongozi huo ulidumu kwa dakika mbili tu baada ya kosa la Declan Rice kupokonywa mpira nje kidogo ya eneo la hatari, Kolo Muani akafunga kwa shuti kali lililomshinda kipa David Raya.
Kipindi cha pili kilianza kwa presha kutoka Arsenal, na dakika ya 47 Jurrien Timber alimpa pasi Gyokeres aliyepata nafasi kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi ya Tottenham na kupiga shuti kali lililomshinda kipa Guglielmo Vicario.
Eze alifunga bao la tatu dakika ya 61 baada ya makosa mengine ya ulinzi wa Spurs, akitumia vyema mpira uliomkuta ndani ya eneo la hatari.
Gyokeres alihitimisha ushindi huo dakika za majeruhi kwa kufunga bao la nne huku mashabiki wa Tottenham wakianza kuondoka uwanjani kwa huzuni.
Ushindi huo umeirejesha Arsenal katika mstari wa mbele wa mbio za ubingwa huku Tottenham wakizidi kusukumwa kuelekea hatari ya kushuka daraja.
