Kamati ya elimu katika bunge la kitaifa limekashfu vikali hatua ya Katibu katika Wizara ya elimu nchini Julius Bitok, kushindwa kufika mbele ya Kamati hiyo kujadili mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028.
Akizungumza baada ya kuhairishwa kwa kikao hicho, Mwenyekiti wa kamati hiyo Julius Melly, alisema kwamba kutofika kwa Katibu huyo  ni dharau kwa kamati hiyo na kunaashiria mwenendo wa kutoheshimu wito wa kamati, akiongeza kwamba sio mara ya kwanza kwa afisa huyo kushindwa kufika au kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu masuala nyeti yanayohusu sekta ya elimu.
Kamati hiyo ilisema kuwa ilitoa mwaliko rasmi kwa Makatibu wote husika kufuatia kuwasilishwa kwa taarifa ya sera ya bajeti bungeni tarehe 11 Februari, ikionyesha wazi tarehe, mahali na ajenda ya kikao hicho kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma.
Ingawa maafisa wengine waliomba udhuru kupitia njia rasmi na wakaruhusiwa, Bitok hakufika wala kutoa maelezo ya kuridhisha, hali iliyolazimu kamati kusubiri baada ya kukamilisha kikao cha awali na Tume ya kuwaajiri Walimu nchini TSC.
Sasa kamati hiyo ilitoa wito rasmi wa kumtaka afike mbele ya kamati hiyo ikionya kuwa endapo hatahudhuria hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Melly alisema kamati haitavumilia dharau kwa Bunge wala uzembe katika kushughulikia masuala yanayogusa sekta muhimu nchini haswa elimu.
Wabunge walisema kutofika kwa Bitok kumechelewesha majadiliano kuhusu changamoto muhimu zinazoikumba sekta ya elimu, zikiwemo msongamano wa wanafunzi shuleni, changamoto za mpito wa wanafunzi kwenye mtaala wa CBE, ukosefu wa bima kwa wanafunzi, ucheleweshaji wa fedha za ruzuku, na hali ya jumla ya usimamizi wa shule.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
