Swazuri afikishwa Mahakamani kwa tuhma za ufisadi

Swazuri afikishwa Mahakamani kwa tuhma za ufisadi

Mahakama ya kuu jijini Nairobi imesikiliza kesi ya ufisadi inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Ardhi (NLC), Prof Mohammad Swazuri, pamoja na washukiwa wengine 16.

Upande wa mashtaka umekuwa na nafasi ya kumhoji Swazuri kuhusu sakata ya ufisadi ya ulipaji fidia kwa waathiriwa wa mradi wa reli ya kisasa SGR wakati akiwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.

Swazuri pamoja na wenzake 16 wanadaiwa kupanga njama ya kutekeleza ufisadi wa takriban shilingi milioni 220, fedha ambazo zilitengwa kulipa fidia waathiriwa wa mradi wa SGR ili ardhi zao zichukuliwe kwa ajali ya mradi huo.

Kulingana na uchunguzi uliyofanywa na idara ya upelelezi na kuwasilishwa Mahakamani, ulibaini kwamba kampuni binafsi ya Dasahe Investments na Olomotit Estate Limited, zililipwa fidia kwa njia isiyo halali licha ya madai kuwa ardhi husika ilikuwa mali ya umma.

Akijitetea mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Eunice Nyutu, Swazuri alijitenga na sakata hiyo akidai kwamba ni shtuma anazoelekezewa ni njama za kumchafulia jina na kumsambaratisha kisiasa, akiweka wazi kwamba hajawahi husika na sakata hiyo ya ufisadi.

Kesi hiyo itaendelea siku ya Ijumaa katika Mahakama hiyo.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi