Rais William Ruto amewaagiza wanafunzi wote wa gredi ya 10 ambao hawana karo ama sare za shule kuhakikisha wanaripoti shuleni kuanzia hapo kesho siku ya Ijumaa.
Rais Ruto alisema serikali kupitia Wizara ya Elimu nchini imesambaza shilingi bilioni 44 shuleni, fedha ambazo zitatumika kufanikisha shughuli mbalimbali za masomo pamoja na matumizi ya shule.
Kiongozi wa taifa, aliwaagiza pia maafisa tawala ikiwemo Machifu na manaibu wao kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kikamilifu ili kufanikisha mpango wa serikali wa kuhakikisha asilimia 100 ya wanafunzi wanahudhuria masomo shuleni.
“Naagiza hakuna mtoto anafaa kusalia nyumbani kwa sababu hakuna karo ya shule, watoto wote waende shule kwa sababu tumetuma pesa bilioni 44 kusomesha watoto wetu na walimu kutekeleza shughuli za masomo, kwa hivyo machifu na manaibu wao wasaidie kuhakikisha watoto wote wanaenda shule, wawe na karo ama hawana ni lazima waende shule”, alisema rais.
Kauli yake imejiri baada ya idadi kubwa ya wazazi kulalamikia kuhangaishwa shuleni kutokana na changamoto za usajili wa wanafunzi pamoja na ukosefu wa karo za shule.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
