Serikali imehakikishia wakaazi wa kaunti 23 nchini ambazo zinakabiliwa na makali ya ukame kwamba inachakula cha kutosha cha kuwawezesha kukabiliana na makali ya njaa.
Akizungumza katika kaunti ya Tanariver baada ya kuongoza ugawaji chakula kwa waathiriwa, waziri wa utumishi wa umma Geoffrey Ruku, alisema hakuna mkenya atakayeaga dunia kwa kukosa chakula.
Waziri Ruku alisema msaada wa chakula hicho ni kwa ajili ya familia zisizo na uwezo katika jamii huku akiwataka maafisa wa utawala wa mkoa kutoa ripoti kuhusu walagahai wa chakula cha msaada.
Wakaazi wa maeneo ya Tanariver wameitaka serikali kubuni mikakati ya Kukabiliana na athari za kiangazi vile vile mafuriko.
Wakati huo huo mbunge wa Garsen katika kaunti ya Tanariver Ali Wario alishinikiza serikali kuu kuongeza mgao wa chakula kwa familia zinazoishi maeneo yanayokabiliwa na makali ya njaa.
Wario alisema msimu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unakaribia na familia zilizoathirika na ukame na mafuriko zinafaa kuzingatiwa hata na zaidi upande wa msaada wa chakula.
Wario alibainisha kuwa usalama wa chakula unafaa kupewa kipaumbele hasa kwa jamii maskini ili kuepusha mahangaiko na maafa.
Taarifa ya Joseph Jira
