Murkomen, awataka machifu na polisi kupambana na pombe haramu

Murkomen, awataka machifu na polisi kupambana na pombe haramu

Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amewataka machifu na manaibu wao kuongeza juhudi katika vita dhidi ya pombe haramu na matumizi ya dawa za kulevya.

Waziri Murkomen alisema kuwa biashara na matumizi ya pombe haramu pamoja na dawa za kulevya vinaendelea kudhoofisha afya ya umma, usalama na utulivu wa kijamii nchini.

Akizungumza katika eneo la Cherangany kaunti ya Trans Nzoia, Murkomen alisema kuwa mapambano dhidi ya pombe haramu na mihadarati yanahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya serikali ya kitaifa, kanisa na jamii kwa ujumla.

“Tuko na jukumu kama serikali ya kitaifa kuhakikisha tunakomesha uuzaji wa pombe haramu na mihadarati kwa ushirikiano wa pamoja na makanisa na jamii kwa sababu hii biashara inafanyika sana mashinani na sasa ndio tunasema ni lazima tukomeshe hii biashara kabisa”, alisema Waziri Murkomen.

Waziri Murkomen katika kikao cha kiusalama na machifu na maafisa wa usalama

Aidha alisisitiza kuwa wasimamizi wa ngazi ya mashinani wana jukumu muhimu katika kusimamia sheria na kulinda jamii dhidi ya madhara ya bidhaa hizo haramu.

Waziri huyo alibainisha kuwa kaunti ya Trans Nzoia ni miongoni mwa kaunti zinazoongoza kwa visa vya pombe haramu na matumizi ya dawa za kulevya, hali aliyosema haikubaliki kamwe.

Taarifa ya Joseph Jira