Maafisa 8 wa polisi wajeruhiwa Garissa

Maafisa 8 wa polisi wajeruhiwa Garissa

Takriban maafisa wanane wa polisi wamejeruhiwa kwenye shambulizi la kigaidi ambapo gari walilokuwa wakisafiria kukanyaga kilipuzi katika barabara ya Banabs-Yumbis kaunti ya Garissa.

Duru kutoka idara ya polisi zilisema kundi la maafisa hao walikuwa wakisafiri kutumia gari la kijeshi lenye uwezo wa kuhimizi mabomu- Mine Resistant Ambush Protected (MRAP) wakati wa tukio hilo.

Hii ni baada ya kikosi cha maafisa wa kuweka usalama mipakani kukabiliana kwa risasi na washukiwa wa ugaidi wanaoaminika kuwa wanamgambo wa kundi la alshabab.

Magaidi hao wanaaminika waliweka bomu la kutegwa ardhini.

Taarifa hiyo ilisema gari la polisi aina ya Land Cruiser lililokuwa na maafisa zaidi limefika eneo la tukio kuwaokoa maafisa wenzao ambao walikuwa wamekwama ndani ya gari hilo la MRAP.

Maafisa hao wamepata majeraha mabaya na kupelekwa katika hospitali iliyokaribu kwa matibabu ya dharura ambapo baadaye watafasirishwa kwa ndege hadi jijini Nairobi.

Polisi eneo hilo wamesema magaidi wamefanikiwa kutoroka eneo la tukio japo wakiibua hofu kuwa huenda wako karibu na eneo hilo linalokabiliwa na tishio la usalama.

Mpaka wa Kenya na Somalia unasalia kuwa hatari na imekuwa rahisi kwa magaidi kupenya nchini.

Taarifa ya Joseph Jira