Maafisa wa Usalama wamenasa shehena ya Bangi katika daraja la Sabaki, Mjini Malindi Kaunti ya Kilifi, iliyokuwa imefichwa kwenye makasha ndani ya basi lililokuwa likisafiri kitoka Lamu kwenda Mombasa.
Basi hilo lilisimamishwa na Maafisa wa usalama katika kizuizi Cha Polisi kilichoko daraja hilo kwa shughuli ya kawaida ya ukaguzi wa magari na mizigo, ambapo magunia mawili ya bangi hiyo yalipatikana yamefichwa katika sehemu ya Mizigo ndani ya basi hilo.
Dereva na Kondakta wa basi hilo, mali ya kampuni ya mabasi ya Tawakal, walikamatwa, ingawa abiria anayeaminika ndiye mwenye kusafirisha bangi hiyo alitotoka mtego huo na bado anatafutwa na Maafisa Polisi.
Waliokamatwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Mjini Malindi huku uchunguzi zaidi unapoendelea.
Maafisa hao wanasema, walipata vidokezo kuhusiana na bangi hiyo ambayo bado haijajulikana thamani yake.
Katika siku za hivi karibuni, Daraja hilo la Sabaki limekuwa chini ya oparesheni kali ya maafisa wa usalama kutokana kuongezeka Kwa idadi ya vyombo vya usafiri, hasa Malori ambayo yaaminika kutumika kwa zaidi kwa biashara haramu kutoka Kaunti za Tana River na Lamu kuingia Kaunti za Kilifi na Mombasa.
Dereva huyo na Kondakta wake watafikishwa mahakamani hivi karibuni huku maafisa wa Polisi wakitia wito kwa wanachi kutoa habari zitakazosaidia kumtia nguvuni mshukiwa mkuu.
