Sports
Mwanariadha Fred Kerley Kukata Rufaa Uamuzi Wa Chama Cha Raidha Duniani
Mshindi wa medali ya shaba ya mbio za mita 100 kwenye Michezo ya Olimpiki na bingwa wa dunia wa mwaka 2022, Fred Kerley, ambaye Jumanne alisimamishwa na Kitengo cha Uadilifu wa Riadha (AIU) kwa kosa la kukosa kuwasilisha taarifa za mahali alipo, ametoa taarifa akitangaza nia yake ya kupinga tuhuma hizo.
Katika taarifa yake, Kerley alisema anaamini kwa dhati kuwa moja ya vipimo vya ghafla anavyodaiwa kukosa inapaswa kuondolewa—ama kwa sababu hakuwa na uzembe wowote au kwa kuwa Afisa wa Udhibiti wa Dawa za Kulevya hakuchukua hatua zinazostahili, kulingana na hali iliyokuwapo, kumtafuta katika eneo alilokuwa ameorodhesha.
Kerley aliongeza kuwa kwa sasa hatatoa maoni zaidi “kwa heshima ya mchakato unaoendelea,” na anatarajia kuwasilisha utetezi wake mbele ya jopo la kusikiliza shauri hilo.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mwanariadha huyo kujiondoa kwenye Mashindano ya Riadha ya Marekani yaliyofanyika Oregon, hali iliyomnyima nafasi ya kushiriki Mashindano ya Dunia yatakayofanyika Tokyo mwezi Septemba mwaka huu.