Business

Muungano wa bodi za leseni za vileo wapinga sera ya NACADA

Published

on

Muungano wa bodi za kudhibiti na kutoa leseni za vileo nchini umepinga vikali pendekezo la Sera ya Mwaka 2025 ya Mamlaka ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA), wakidai kuwa linaenda kinyume na ugatuzi na kuondoa mamlaka ya kikatiba ya serikali za kaunti katika usimamizi wa biashara ya vileo.

Wakizungumza mjini Diani kaunti ya Kwale, wanachama wa Muungano huo wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Julius Owino, walisisitiza kuwa serikali za kaunti ndizo zenye jukumu la kisheria na kikatiba la kutoa leseni, kusimamia, na kutekeleza sheria zinazohusu uuzaji wa pombe.

“Sera hii ya NACADA ni jaribio la kuingilia majukumu ya kaunti na itaathiri mapato ya serikali za kaunti, kaunti lazima zisalie na mamlaka kamili ya kusimamia biashara ya vileo kama ilivyowekwa katika Katiba,” alisema Owino.

Owino pia aliitaka NACADA kushirikiana na kaunti kwa njia ya mashauriano badala ya kujaribu kuchukua majukumu yao, akiongeza kuwa ushirikiano thabiti ndio utaleta mafanikio katika udhibiti wa pombe na dawa za kulevya.

Kauli yake iliungwa mkono na Richard Osongo, Mwenyekiti wa wamiliki wa baa katika kaunti ya Kwale, ambaye alitoa onyo kali dhidi ya kile alichokiita “unyanyasaji wa mamlaka za kaunti na NACADA.”

Muungano huo ulieleza kuwa utatoa mapendekezo rasmi kwa serikali ya kitaifa na kuhimiza mjadala wa wazi kabla ya utekelezaji wowote wa sera hiyo mpya.

Taarifa ya Elizabeth Mwende

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version