County

Mung’aro Awaonya Madaktari na wahudumu wa Afya Wenye Hulka ya Kuiba Dawa Hospitalini

Published

on

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro amewaonya madaktari na wahudumu wengine wa afya katika kaunti hiyo wenye hulka ya kuiba madawa hospitalini, akisema kwamba watakaopatikana watakabiliwa kisheria.

Akizungumza baada ya kuzindua kitengo cha Radiolojia katika jengo la Kilifi County Medical Complex, Gavana Mung’aro amesema tangu aingie uongozini Serikali yake imefanikiwa kuwakamata wale ambao wamekuwa wakihusika na wizi wa madawa hospitalini.

Kiongozi huyo amesema serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na wadau wengine wanaendeleza mikakati ya kuhakikisha hospitali na zahanati za umma katika kaunti hiyo zinakuwa na vifaa vya kisasa vya matibabu.

“Nilipoingia kama Gavana nilianza kusafisha hii kaunti kwa sababu tulipokuwa walikuwa wengi sana lakini inakaa bado wako kwamba watu wanalipa pesa na watu wanapeleka pesa kwa akaunti zao ama wanatengezewa liseni bandia apewe na watu wachukue pesa waeke mfumo, nataka kuwahakikisha kwamba siku chache zijazo nitangaza watu wengi sana ambao wataenda nyumbani,” Gavana Mung’aro.

Kwa upande wake Naibu Gavana wa kaunti hiyo Flora Chibule amesema ushirikiano zaidi utaendelezwa, kati ya serikali ya kaunti na wadau wengine ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa ipasavyo.

Ameahidi kumuunga mkono Gavana Mung’aro kufanikisha juhudi bora za utoaji wa huduma kwa wakaazi wa kaunti ya Kilifi, akisema hiyo ndio hatua pekee ya kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi ya maendeleo.

“Sisi tuko nyuma yake kumuunga mkono na kwa yeyote yule ambaye ataingia kwa siasa hayo ni ya 2032 lakini tugange haya ya leo ya kwamba siku hii ya leo tunafurahikia tuna mashine ya kufanya ukaguzi wa kiafya,” Chibule.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version