News
Maseneta wamtaka Murkomen na Kanja kujiuzulu
Maseneta katika bunge la Seneti wamemtaka Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja kueleza kilichosababisha kifo cha mwanablogu Albert Ojwang aliyefariki katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi.
Wamemtaka Murkomen kueleza umma kwa nini taarifa zilizotolewa na Kanja kuhusu kisa hicho zinakinzana na ripoti iliyotolewa na mwanapatholojia wa serikali Benard Midia baada ya kuufanyia upasuaji mwili wa Ojwang.
Akichangia hoja hiyo katika vikao vya bunge la Seneti, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amemtaka Waziri Murkomen kujiuzulu akidai kwamba amezembea katika utendakazi wake huku akimtaka Inspekta Kanja kuwaomba wakenya msamaha sawa na familia ya Ojwang’ haki inapatikana.
“Bwana Spika wazalendo wa nchi hii walipigana dhidi ya kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka na Waziri Murkomen ninakuhakikishia kwamba watapigana dhidi ya mauaji ya kiholela hasa wakiwa chini ya ulinzi wa polisi. heshima ya kijana huyu tafadhali wewe bado hujakuza mtoto hadi umri wa miaka 31, tafadhali si ya kibinafsi unaweza kujiuzulu mara moja kwani umeonyesha wazi haufai kushikilia wadhfa huo”, alisema Seneta Boni Khalwale.
Vikao hivyo hata hivyo vimeibua maswali mengi kuhusu mauaji ya kiholela na utekaji nyara nchini.
Taarifa ya Elizebeth Mwende