News
Mackenzie yuko salama, wasema maafisa gerezani Shimo la tewa
Afisa anayesimamia gereza la Shimo la Tewa, Abdi Willy Adan amekanusha madai yalioibuliwa na mhubiri tata Paul Mackenzie kwamba maisha yake yako hatarini akiwa katika gerezani hilo.
Akizungumza mbele ya mahakama ya watoto ya Tononoka, Adan alisema hakuna vitu vya kutiliwa shaka vilivyowekwa kwenye chumba cha Mackenzie katika gereza hilo la Shimo la Tewa, na kwamba usalama wa gereza uko imara.
Mackenzie, anayekabiliwa na mashtaka yanayohusiana na mauaji ya Shakahola, alikuwa ameomba kuhamishwa hadi Gereza la Manyani lakini Adan alikataa, akisema uzito wa mashtaka unahitaji asalie katika gereza la usalama wa juu.
Adan Pia alisema madai ya Mackenzie ya mgomo wa njaa hayana msingi wowote kwani rekodi zinaonyesha wazi kwamba yeye na washukiwa wengine wanaendelea kula chakula wakiwa gerezani.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Jami Yamina, ulipinga ombi la kuahirisha kwa kesi hiyo kwa sababu ya mgomo wa njaa, na kuutaja kama jaribio la kuchelewesha haki ya waathiriwa.
Hata hivyo Hakimu Nelly Chepchirchir alikataa ombi la kuahirisha kwa kesi hiyo, akisema mgomo wa njaa wa kujiletea sio sababu ya kusimamisha kesi, na akaagiza washukiwa wapewe nafasi ya kuwasiliana na mawakili wao.
Mackenzie na wenzake 34 wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya watoto katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu