Sports
Mabondia Wawili Wafariki Nchini Japan Baada ya Mapigano Tofauti
Mabondia wawili nchini Japan wamefariki dunia baada ya kupata majeraha makubwa katika mapigano mawili tofauti yaliyofanyika jijini Tokyo wikendi hii.
Bondia wa uzani wa Super Featherweight, Shigetoshi Kotari, na mwenzake Hiromasa Urakawa, wote wakiwa na umri wa miaka 28, walikimbizwa hospitalini baada ya kupoteza fahamu katika mapigano yao tofauti.
Wanabondia hao walihitaji kufanyiwa upasuaji wa ubongo, lakini hata hivyo walipoteza maisha wakiwa hospitalini.
Kotari alipoteza fahamu wakati wa pambano lake dhidi ya Yamato Hata, na licha ya juhudi za madaktari baada ya kukimbizwa hospitalini, alifariki saa nne usiku.
Urakawa naye alipoteza fahamu katika raundi ya nane ya pambano lake dhidi ya Yoji Saito. Pigano hilo lilikatishwa na alihamishiwa hospitalini, ambako alifariki usiku wa Jumamosi.
Chama cha Mabondia nchini Japan kilitoa salamu za rambirambi, na kupitia kwa Mkurugenzi wake Mtendaji Tsuyoshi Yasukochi, kilieleza masikitiko makubwa, kikisema kuwa hii ni mara ya kwanza katika historia ya mchezo huo nchini humo kwa mabondia wawili kupoteza maisha ndani ya kipindi kimoja.