News
Lung’anzi, alaumu viongozi wa Kwale kwa kutowajibika
Mwanasiasa na Mfanyibiashara Lung’anzi Chai amelalamikia huduma duni mashinani zinazotolewa na viongozi walio mamlakani kaunti ya Kwale, akisema wakaazi wengi wamekuwa wakihangaika kwa kukosa huduma bora.
Akizungumza na Wanahabari katika kaunti ya Kwale, Lung’azi alisema japo serikali ya kaunti ya Kwale imetenga fedha kwa Wawakilishi wadi kufanikisha huduma za maendeleo mashinani, bado wananchi wanakosa huduma hizo.
Lung’anzi alisema huduma kama zile za afya zimekuwa za kujikokota kwani baadhi ya vituo vya afya havina madawa na vifaa vya matibabu, hali ambayo imewafanya wananchi wengi kugharamika zaidi.
Mwanasiasa huyo hata hivyo alijitenga na madai kwamba huenda akamuunga mkono mwanasiasa mwengine katika kuwania kiti cha ugavana wa Kwale wakati wa uchaguzi mkuu ujao, akisema tayari ametangaza msimamo wake.
“Mgao umeongezwa na wale wenzetu ambao wako kwenye madaraka kufikia milioni 25 kila wadi lakini bado huduma mbalimbali muhimu zimekosa kufika mashinani licha ya serikali kuwa na uwezo wa kufanikisha maendeleo, hospitali nyingi hazina madawa na vifaa bora vya matibabu”, alisema Lung’anzi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.