Sports
Kocha wa Stars Benni Mccarthy Ana Imani Kupata Ushindi dhidi ya Madagascar Robo Fainali CHAN Kasarani
Kocha mkuu wa Harambee Stars, Benni McCarthy, ameonyesha imani kubwa huku kikosi chake kikijiandaa kwa pambano la kihistoria la robo fainali dhidi ya Madagascar litakalochezwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani, Ijumaa, Agosti 22 saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kabla ya mechi akiwa ameandamana na nahodha msaidizi Daniel Sakari, McCarthy amesema safari ya Stars katika hatua ya makundi imewaimarisha kwa hatua ya muondoano.
Kenya iliongoza katika kundi gumu lililojumuisha DR Congo, Angola, Morocco na Zambia na kufanikisha tiketi ya kufika robo fainali.
“Baada ya mtihani tulioupitia hatua ya makundi, nafikiri hakuna timu ambayo tunaogopa tena. Fursa zetu zilikuwa finyu, lakini tulijithibitisha kwamba tuna uwezo wa kuvuka vikwazo hivyo. Yeyote atakayekuja mbele yetu atakuwa changamoto nzuri, lakini mtazamo wetu ni sisi wenyewe na kusonga hatua inayofuata,” alisema McCarthy.
Mtaalamu huyo kutoka Afrika Kusini alibainisha maandalizi yake yanahusisha zaidi ya mbinu, akisisitiza uimara wa kisaikolojia.
“Nafanya kazi ya kujenga utulivu wa kiakili ndani ya wachezaji wangu. Matumaini yako juu, lakini tulifanya uchambuzi wetu wa wapinzani watarajiwa. Madagascar watakuwa kizuizi kingine, na haijalishi tulichokipata kabla, kimesahaulika. Tunapaswa kujiandaa kadiri tuwezavyo,” alisisitiza McCarthy.
McCarthy alithibitisha kuwa hakuna majeraha makubwa kuelekea robo fainali. Mchezaji pekee atakayekosa ni Chrispine Erambo, aliyesimamishwa baada ya kadi nyekundu wakati wa ushindi wa Stars wa 1-0 dhidi ya Morocco.
Akitambua ubora wa kipa Byrne Omondi aliyeibuka shujaa wa mechi, McCarthy aliwataka wachezaji wake kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji.
Ushindi dhidi ya Madagascar utaipeleka Kenya kwenye nusu fainali dhidi ya mshindi kati ya Algeria na Sudan watakaovaana Jumamosi, Agosti 23, kule Zanzibar.