Sports
Kocha Ngao Ajitolea Kukuza Taekwondo Kaunti ya Kilifi Kupitia Legends Cup
Mwanzilishi wa kombe la Legends Cup na kocha wa mchezo wa Taekwondo, Onesmas Safari Ngao, amesema kuwa lengo lake kuu ni kuinua viwango vya mchezo huo ambao umekuwa ukidorora katika Kaunti ya Kilifi.
Akizungumza katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Pwani, ambako zaidi ya wanataekwondo 50 walijitokeza kuonyesha uwezo wao, Kocha Ngao alieleza kuwa licha ya Taekwondo kudorora kwa muda mrefu katika kaunti hiyo, sasa yuko tayari kufufua ari na ubora wa mchezo huo, na kuwapa nafasi vijana kuonyesha uweledi na vipaji vyao.
Kwa upande wake, mchezaji Shukrani Chai, ambaye aliondolewa katika hatua ya nusu fainali, alisifia kurejea kwa mashindano kama haya, akisema ni hatua muhimu ya kukuza viwango vya mchezo huo Kilifi, huku akimshukuru Kocha Ngao kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwapa vijana fursa.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Rehema Furaha, ambaye aliongeza kuwa kurejea kwa Kocha Ngao katika medani ya Taekwondo kunawapa motisha na ari mpya ya kujituma katika mchezo huo.
Washindi katika vitengo mbalimbali walituzwa kwa vikombe, medali, na vyeti vya ushiriki, kama njia ya kutambua na kuhamasisha juhudi zao.