News
Kesi ya Pembe za Ndovu kuendelea katika Mahakama ya Mombasa
Raia wawili wa taifa la Burundi wamefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya kumiliki na kujaribu kusafirisha pembe za Ndovu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 12.
Gakiza Sulemani na Nkunubumwe Celecius walifikishwa mbele ya Hakimu mkaazi Mwandamizi David Odhiambo kwa makosa ya kushughulikia vipande 27 vya pembe za Ndovu kinyume cha sheria.
Pembe hizo zilizokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 62.85, zilinaswa katika eneo la Miritini kaunti ya Mombasa kufuatia operesheni ya kijasusi iliyotekelezwa na maafisa wa Huduma ya Wanyamapori nchini KWS.
Washukiwa hao pia walikabiliwa na shtaka la pili la kumiliki sehemu za wanyamapori walioko kwenye hatari ya kutoweka bila idhini ya serikali kinyume na sheria ya mwaka 2013.
Washukiwa hao hata hivyo walikana mashtaka hayo huku Mahakama ikiwaachilia kwa dhamana ya shilingi milioni 4 kila mmoja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho pamoja na masharti ya kuwasilisha pasipoti zao na majina ya Wakenya wawili wa kuwawajibikia.
Kesi hiyo itatajwa tena mnamo tarehe 20 mwezi huu Agosti.
Taarifa ya Mwanahabari wetu