News
Joho atangaza kuwania urais siku zijazo
Waziri wa madini na masuala ya bahari nchini Hassan Ali Joho, alidokeza kwamba katika siku zijazo eneo la Pwani litatoa rais wa taifa la Kenya.
Waziri Joho aliwataka wakaazi wa Pwani kutojiingiza katika mivutano ya kisiasa na mirengo mingine ya kisiasa nchini, akisema ni wakati mwafaka wa wapwani kuungana na kujipanga kisiasa.
Waziri Joho alisema mtu ambaye alikuwa na nafasi nzuri ya kushikilia wadhfa huo wa kitaifa aliyekuwa ni Marehemu Karisa Maitha lakini ndoto hiyo bado ipo, akiweka wazi kwamba anamezea mate kiti hicho katika siku zijazo.
“Mara ya kwanza nilifikia kama kuna mpwani anaweza kuwa rais ilikuwa ni marehemu Karisa, lakini mimi hiyo ndoto bado niko nayo na nina imani iko siku bado hapa Pwani kuzaa rais. Siku moja wataskia rais Hassan na nikujipanga”, alisema Joho.
Joho alisisitiza haja ya wapwani kujipanga kisiasa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kuvuna kwenye ngazi ya kitaifa pamoja na kuwa rahisi kwa eneo la Pwani kuwania kiti hicho na kutangaza rais wa Kenya katika siku zijazo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi