Huduma za matibabu katika hospitali na zahanati za umma kaunti ya Kilifi zimerejea kama kawaida baada ya wauguzi waliokuwa katika mgomo kusitisha mgomo wao rasmi.
Hii ni baada ya kikao cha siku nzima kati ya serikali ya kaunti ya Kilifi ikiongozwa na Gavana Gedion Mung’aro na viongozi wa Muungano wa wauguzi kaunti ya Kilifi wakiongozwa na Katibu mkuu wa Muungano huo wa wauguzi Derrick Abdallah ambapo waliafikia kutekelezwa kwa mkataba wa makubaliano wa malipo CBA.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kikao hicho cha maafikiano, Gavana Mung’aro alisema masuala yote yalioibuliwa na wauguzi hao yatatelezwa kwa kuambatana na sheria sawa na kubuniwa kwa jopo maalum litakaloogozwa na Waziri wa Afya kaunti ya Kilifi Peter Mwarogo kutatua masuala yaliyosalia.
“Tumekuwa na kikao cha siku nzima na wauguzi wa Kilifi na mnajua kwamba walikuwa kwa mgomo wa kitaifa lakini kama kaunti ya Kilifi tumekubaliana kutekeleza masuala kadhaa waliyokuwa nayo ili kurejea kwa huduma za afya katika mkataba wa CBA na tumesema tutabuni kamati kati ya bodi ya huduma za umma na Waziri wa afya Peter Mwarogo na wauguzi kutatua masuala yaliyosalia”, alisema Gavana Mung’aro.
Gavana Mung’aro aliweka wazi kwamba barua zilizoandikwa kwa wauguzi 21 zimefutiliwa mbali, akisema watapewa barua zingine za kurejea kazini huku akionya kwamba ni lazima wauguzi kuzingatia sheria na nidhamu.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Muungano wa wauguzi hao kaunti ya Kilifi Derrick Abdallah aliwaagiza wauguzi wote waliokuwa katika mgomo kurejea kazini katika mda wa masaa 24, akisema masuala yote ibuka ikiwemo mishahara yatatauliwa.
“Tunawahimiza wauguzi kurejea kazini katika muda wa saa 24, zile barua zilizotumwa kwa wauguzi tumeelewa zitafutiliwa mbali na leo gavana ameahidi kuongeza shilingi elfu tano katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025 ya sare za kazi na masuala mengine muhimu pia tumeafikiana.”, alisema Derrick.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi