Sports
Harambee Stars Kuvaa Angola Jioni ya Leo Kusaka Alama Tatu Muhimu CHAN
Timu ya taifa ya soka, Harambee Stars, itashuka dimbani jioni ya leo kuwania alama tatu muhimu dhidi ya Angola, katika mechi yao ya pili ya mashindano ya CHAN kwenye Uwanja wa Kasarani.
Kocha wa Harambee Stars amekiri kuwa haitakuwa mechi rahisi, lakini ana imani kuwa kikosi chake kiko tayari kwa kibarua hicho kigumu.
“Angola walicheza vizuri dhidi ya Morocco. Walikuwa na zaidi ya mashuti 10 golini mwa wapinzani wao, lakini walishindwa kufunga. Niliwaangalia wakicheza — ni timu inayounda nafasi nyingi, hivyo si wapinzani wa kubeza hata kidogo licha ya kupoteza mechi yao ya kwanza,” alisema kocha huyo.
Katika taarifa nyingine, kocha huyo amefichua kuwa mshambulizi Masoud Juma huenda akaukosa mchuano wa leo kufuatia jeraha alilopata kwenye mechi dhidi ya DR Congo. Hali yake bado ni ya mashaka huku akisubiri tathmini ya mwisho kutoka kwa madaktari wa timu.
“Masoud alipata kugongwa dhidi ya DR Congo na kwa sasa hali yake haijaridhisha. Madaktari watatupa taarifa ya mwisho, lakini inaelekea hatacheza mechi ya leo. Kwa upande mwingine, Manzur Suleiman amepona jeraha lake na yuko tayari kuanza mechi hiyo,” aliongeza.
Harambee Stars wanatarajiwa kushuka uwanjani saa moja usiku, kabla ya pambano la awali kati ya Zambia na DR Congo litakalopigwa saa kumi na mbili jioni.