News
Fikirini: Ni sharti vijana wapewe nafasi na fursa za kiuchumi
Katibu katika Wizara ya vijana na uchumi bunifu nchini Fikirini Jacobs amesema juma la vijana limebuniwa ili kutoa nafasi zaidi kwa vijana wengi kuwasilisha matakwa yao kwa idara husika kinyume na kusherehekea siku moja tu ya kimataifa ya vijana.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa maadhimisho ya juma la vijana katika chuo kikuu cha Pwani, Fikirini alisema kuwa siku moja haitoshi kwa vijana wote nchini kupata fursa ya kuwasilisha hoja zao kwa viongozi.
“Katika juma hili la vijana Wizara ya vijana na uchumi bunifu itazuru maeneo mengine ya taifa huku kilele cha sherehe za siku ya vijana ulimwenguni ambayo itakuwa tarehe 12 zikitarajiwa kuadhimishwa katika chuo kikuu cha Masinde Muliro”, alisema Fikirini.
Fikirini alikariri kuwa vijana wengi wana matakwa mengi ya kuyawasilisha hivyo wanapaswa kutengenezewa majukwaa mbalimbali ya kutoa maoni yao.
Aidha Fikirini aliwashauri vijana kutumia mitandao kama chombo cha kujiimarisha kiuchumi badala ya kuitumia kwa maswala yasiofaa.
Ni hafla ambayo iliongozwa na Naibu rais Prof. Kithure Kindiki, Waziri wa Michezo nchini Salim Mvurya, mbunge wa Kilifi kaskazini, Owen Baya, Mwakilishi wa kike kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu, Mwenyekiti wa bodi ya barabara nchini Aisha Jumwa miongoni mwa viongozi wengine.
Mamia ya vijana kutoka kaunti ya Kilifi walijumuika kwenye uzinduzi wa maadhimisho hayo sawa na baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Pwani.
Taarifa ya Hamis Kombe