News
Familia ya mchuuzi aliyepigwa risasi Nairobi yalilia haki.
Familia ya Boniface Mwangi Kariuki, mchuuzi mwenye umri wa miaka 22 aliyepigwa risasi kichwani na afisa wa polisi wa kupambana na ghasia katika barabara ya Moi jijini Nairobi wakati wa maandamano sasa inaomba haki na hatua za haraka zichukuliwe.
Jonah Kariuki Nyambura babake mwathiriwa alidai hakufahamu kosa la mwanawe lililomfanya afisa wa polisi kufyatua risasi akisema alikuwa akijilinda tu kwa kuuza barakoa.
Akihutubia wanahabari Jumatano asubuhi 18 juni 2025, Nyambura alisema mwanawe yuko katika hali mahututi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), alikopelekwa kutibiwa baada ya kupata majeraha mabaya kichwani.
Kariuki aliongeza kuwa alifarijika baada ya kumuona mtoto wake akiwa hai, kinyume na taarifa za awali kuwa alifariki baada ya kupigwa risasi.
“Nilimuona kwenye video hiyo kwenye simu yangu, na majira ya saa nane jioni nilipigiwa simu na watu wake wa karibu kuwa mwanangu amepigwa risasi, nililala hapa (KNH) na asubuhi nilimuona katika chumba cha wagonjwa mahututi- ICU, angalau sasa nina matumaini,” alisema Kaiuku.
Aidha aliomba hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya afisa wa polisi aliyempiga risasi mwanawe.
“Ningewaomba maafisa wa polisi wawajibike kwa sababu wana watoto pia. Aliyempiga risasi pia ni mtoto wa mtu. Hatua kali zichukuliwe dhidi ya afisa huyo wa polisi,” aliongeza Kariuki.
Alikuwa ameandamana na seneta wa Busia Okiya Omtatah, ambaye alilaani ukatili wa polisi, na kuongeza kwamba tukio hilo lazima lishughulikiwe haraka.
Wakati huo huo huduma ya kitaifa ya Polisi NPS ilithibitisha kukamatwa kwa afisa aliyempiga risasi Mwangi huku shinikizo la kudhibiti ukatili wa polisi nchini likiendelea kukithiri.
Kwa upande wake rais wa chama cha mawakili Faith Odhiambo ametoa wito wa kukamatwa kwa afisa mwengine wa polisi aliyeonekana kwenye video na afisa wa polisi aliyempiga risasi mchuuzi wa barakoa kichwani wakati wa maandamano ya Jumanne 17 Juni 2025 jijini Nairobi.
Taarifa ya Joseph Jira