News
Familia 200 Eneo la Msambweni Zavunjiwa Nyumba
Zaidi ya familia 200 katika kijiji cha Gazi eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale zinakadiria hasa ya mamilioni ya pesa baada ya genge la vijana kuvamia makaazi yao na kubomoa nyumba.
Familia hizo zinazoishi kama maskwota katika kipande cha ardhi cha zaidi ya ekari 300, zimelalamikia kuvunjiwa nyumba zao bila ya agizo lolote kutoka kwa idara ya Mahakama nchini.
Wakiongozwa na Nyawa Mwero, familia hizo zinaitaka serikali kuingilia kati swala hilo na kuhakikisha haki inatendeka baada ya nyumba zao kubomolewa na genge hilo la vijana wanaodaiwa kukodishwa ili kutekeleza ubomozi huo.
Familia hizo zimewalaumu pakubwa viongozi wa kaunti ya Kwale baada ya zoezi la ubomozi wa nyumba zao kutekelezwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi kaunti ya Kwale Reginald Omaria amekanusha madai kwamba maafisa wa usalama wanahusika katika ubomozi huo, akisema maafisa hao walikuwa wanatekeleza jukumu la kuimarisha usalama.