News

EACC: Wizara ya Usalama na Afya zaongoza kwa ufisadi

Published

on

Utafiti mpya wa kitaifa uliofanywa na Tume ya maadili ya kupambana na ufisadi nchini EACC umeonya wakenya dhidi ya vitendo visivyo vya kimaadili na ufisadi katika Wizara ya usalama wa ndani na taasisi nyingine za umma.

Kulingana na utafiti wa mwaka 2024 wa tume hiyo, asilimia 47.8 ya wakenya waliotangamana na Wizara ya usalama wa ndani waliripoti kupitia au kushuhudia vitendo vya ufisadi au visivyo vya kimaadili.

Hali hii inaifanya Wizara hiyo kuwa na kiwango kikubwa cha matukio kama haya.

Wizara ya Afya nchini ilishika nafasi ya pili kwa asilimia 19.7, huku hazina ya kitaifa ikifuata kwa mbali kwa asilimia 5.8.

Taasisi nyingine za umma zilizojitokeza kwa wingi ni pamoja na wizara ya Ardhi kwa asilimia 5.6, uchukuzi kwa asilimia 3.9, na elimu kwa asilimia 2.6.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Agosti na Oktoba 2024, uliwashirikisha zaidi ya watu 6,000 kote nchini na ulilenga kuelewa mitazamo na uzoefu wa wananchi kuhusiana na rushwa na maadili katika utumishi wa umma.

Ripoti hiyo ilifichua kuwa wakenya bado wanakabiliana na viwango vya juu vya hongo na tabia isiyofaa katika taasisi za umma.

Pia ilifichua hali inayotia wasiwasi ambapo rushwa inazidi kuonekana kama uovu muhimu katika kupata huduma za umma.

Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa wananchi wengi wanahisi wamenaswa katika mzunguko wa unyang’anyi na kuogopa kudhulumiwa ikiwa watazungumza.

Kaunti ya Nairobi iliongoza orodha ya vitengo vya ugatuzi ambapo wakaazi waliripoti kukabiliwa na visa vya juu zaidi vya ufisadi, ikifuatiwa na Kiambu, Machakos, Kisumu na Nakuru.

Tume hiyo iliwataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika kutoa huduma kwa Wakenya.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version