Sports
Haller Ajiunga Rasmi na Utrecht Baada ya Kuondoka Borussia Dortmund
Kilabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani imethibitisha kwamba mshambuliaji wa taifa la Ivory Coast Sebastien Haller amejiunga na klabu ya Uholanzi, Utrecht, kwa mkataba wa kudumu.
Inaripotiwa kuwa Haller amejiunga kwa uhamisho wa bure baada ya kuruhusiwa kuvunja mkataba wake na Dortmund mwaka mmoja kabla ya muda wake kuisha.
Raia huyo wa taifa la Ivory Coast mwenye umri wa miaka 31 alitumikia nusu ya pili ya msimu uliopita kwa mkopo Utrecht, klabu aliyowahi kuichezea kati ya mwaka 2015 na 2017. Kuondoka kwake kunahitimisha kipindi kigumu akiwa Dortmund.
Baada ya kusajiliwa kwa dau la euro milioni 31 ($36m) kutoka Ajax mwaka 2022, Haller aligunduliwa kuwa na saratani ya korodani wiki chache baadaye na akakaa nje kwa miezi sita akipokea matibabu.
Alikosa penalti katika siku ya mwisho ya msimu wa 2022-23 kwenye sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Mainz, matokeo yaliyoiwezesha Bayern Munich kutwaa ubingwa wa Bundesliga.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa zamani wa West Ham na Eintracht Frankfurt ndiye aliyefunga bao la ushindi kwa Ivory Coast katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana dhidi ya Nigeria.