News

Bunge la kaunti ya Kilifi kujadili hatma ya Spika Mwambire

Published

on

Mswada unaolenga kumuondoa Mamlakani Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire, uliwasilishwa kwa Karani wa bunge hilo Micheal Ngala.

Kulingana na utaratibu wa mabunge ya kaunti, Mswada uliowasilishwa na Mwakilishi wadi wa Tezo Thomas Chengo, utapelekwa kwa ofisi ya Spika ambaye kwa mujibu wa Sheria atauwasilisha kwa kamati ya shughuli za bunge hilo kabla ya kuwasilishwa bungeni ili kujadiliwa.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa bunge hilo kujadili hatma ya Spika Teddy Mwambire.

Miongoni mwa madai yaliyoibuliwa dhidi ya Spika Mwambire, ni pamoja na kuendelea kuhudumu katika wadhfa wake akiwa bado ni Mwenyekiti wa Chama cha ODM kaunti ya Kilifi, kuhujumu serikali ya Gavana Gideon Mungaro katika utekelezwaji wa miradi ya maendeleo miongoni mwa madai mwengine.

Kumekuwa na mpasuko mkubwa katika bunge la kaunti ya Kilifi baina ya Wawakilishi wadi wanaoegemea upande wa Gavana Mungaro na wale wanaokosoa serikali yake.

Picha kwa hisani: Bunge la kaunti ya Kilifi

Akizungumza na CocoFm, Spika Teddy Mwambire alithibitisha kuwasilishwa kwa mswada huu mbele ya Karani wa bunge hilo, japo mswada huo haujawasilishwa ofisini mwake huku akihoji kwamba shtuma hizo dhidi yake hazina msingi wowote.

Hata hivyo alisema atafuata sheria kuhakikisha kwamba mswada huo unazingatia vigezo vyote vya kisheria vya kuwasilisha mswada bungeni na kujadiliwa kikamilifu.

Itakumbukwa kwamba mwezi uliopita vurugu zilishuhudiwa wakati Wawakilishi wadi wakijadili bajeti ya kaunti hali iliyosababisha kushambuliwa kwa Mwakilishi wadi mteule Elina Mapenzi na wenzake wawili Ibrahim Matumbo (Watamu) na Twaher Abdulkarim (Sheila).

Vurugu hizo zilishuhudiwa wakati baadhi ya Wawakikishi wadi wanaoegemea mrengo wa Gavana Mungaro kususia vikao vya bunge vilivyotarajiwa kumhoji Waziri wa Afya kaunti ya Kilifi Peter Mworogo na Katibu wake David Mulewa kwa madai ya usimamizi mbaya wa Wizara ya Afya kaunti ya Kilifi.

Taarifa ya Eric Ponda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version