News
Gataya: Kaunti ya Kilifi Imeonyesha Kuwajibika Kisheria
Kamati ya utekelezaji wa sheria katika bunge la Seneti imefanya kikao na Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mung’aro kutathmini jinsi serikali ya kaunti hiyo inavyoendana na sheria za kitaifa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mwenda Gataya amesema kati ya kaunti ambazo kamati hiyo imezitembelea, serikali ya kaunti ya Kilifi imeonyesha kuwajibika katika kuzingatia sheria.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kikao hicho katika makao makuu ya Gavana wa Kilifi, Gataya ambaye pia ni Seneta wa kaunti ya Tharaka Nithi, amesema hatua hiyo imesaidia kuzuia mivutano ya kisheria.
“Tumefurahishwa na kaunti ya Kilifi jinsi ilivyofuata sheria na katiba na kama kamati ya seneti tumeridhia hatua hiyo kwamba kaunti ya Kilifi ni kati ya kaunti bora zaidi kwa kufata sheria na ndio matarajio yetu. Tumeangalia matumizi ya hazina ya wadi pamoja na zengine na kweli ni wazi kwamba imezingatia sheria kwa kuhusisha umma”, Gataya.
Kwa upande wake Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro amesema wanalenga kubuni sheria itakayowawezesha wasimamizi wa vijiji kutambulika kisheria, sawa na kubuni sheria itakayojumuisha wananchi katika ujenzi wa shule za Chekechea ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha pamoja na kubuni sheria itakayosimamia bodi ya ukusanyaji ushuru wa kaunti.
Wakati huo huo Gavana Mung’aro amedokeza kwamba tangu achukue hatamu ya uongozi, kaunti ya Kilifi imefaulu kurejesha zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kutoka kwa kesi mbalimbali zilizowasilishwa Mahakamani, akisema ni lazima sheria izingatiwe.
“Kuna kesi moja hii kaunti ilikuwa inadaiwa milioni 926 na nikapambana hadi milioni 114, moja ilikuwa bilioni 1.1 na kuenda Mahakamani na tukashinda hiyo kesi na labda wakate rufaa na tupate taarifa kutoka Mahakamani lakini kesi hiyo tulishinda kwa hivyo kaunti imepata bilioni 1.1 pamoja na milioni 800 hiyo ni bilioni 1.9”, Mung’aro.