National News
Marekani Yatoa Tahadhari ya Usafiri kwa Raia wake, Kenya
TAHADHARI-
Taifa la Marekani limetoa tahadhari ya usafiri kwa raia wake, likiwataka kutotembelea maeneo ya mpaka wa Kenya na Somalia kutokana uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi, uhalifu na utekejinyara.
Kupitia Ubalozi wake humu nchini, taifa hilo limetaja kaunti za Mandera, Wajir na Garissa kama maeneo hatari yenye matukio ya kigaidi na kuwashauri raia wake kutotembelea sehemu hizo.
Katika ukanda wa Pwani, ubalozi huo wa Marekani umewatahadharisha raia wake dhidi ya kutembelea maeneo kadhaa ya kaunti ya Kilifi ikiwemo Kaskazini mwa mji wa Malindi na kaunti ya Lamu na Tana River.
Tahadhari hiyo hata hivyo haikutaja mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Tsavo, japo ikafahamisha kaunti za West Pokot na Turkana kama kaunti ambazo ziko katika hatari kutokana na matukio ya uvamizi wa majangili wanaoiba mifugo.
Wakati uo huo Marekani imetahadharisha raia wake kuwa makini wanapotembelea sehemu za Kibera na Eastleigh jijini Nairobi kutokana na ongezeko la visa vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikichangia changamoto kwa maafisa wa usalama kuvikabili.