National News
Washukuwa Wawili wa Kundi la Kigaidi la Alshabab Watiwa Nguvuni
Watu wawili wanaoshukuwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Alshabab wametiwa nguvuni na maafisa wa kupambana na magaidi nchini ATPU katika kaunti ya Mandera.
Kulingana na maafisa hao, mshukiwa mmoja alifaulu kuvuka mpakani kutoka El-Adde nchini Somalia hadi nchini Kenya na kufanikiwa kupata kitambulisho cha kitaifa ili kutimiza malengo ya kigaidi.
Idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI imesema washukiwa hao wawili akiwemo Issac Mohammed Abdi na Noor Yakub Ali wote wakiwa na umri wa miaka 29, walikuwa wamepanga kuwateka nyara raia wa China waliokuwa wakitengeza mabomba ya maji katika uwanja wa ndege wa Mandera.
DCI imesema Mohammed alikuwa amepanga njama na mwandani wake humu nchini kumsaidia kumteka nyara raia wa China kwa gharama ya shilingi elfu laki moja ili kufanikisha mipango ya kusafirisha raia wa China hadi Somalia.
Maafisa hao wamesema baadaye walibaini kwamba gaidi mwengine Noor Yakub Ali, alikuwa amepanga kusaidia usafirisha wa utekaji nyara kwa gharama ya shilingi laki tatu hadi eneo la El-Adde nchini Somalia kabla ya njama hiyo kutibuka.
Washukiwa hao wanaendelea kuzuiliwa na maafisa wa kupambana na magaidi nchini ATPU kwa uchunguzi zaidi.