News
Upasuaji wa maiti wagundua vipande 4 vya risasi kichwani.
Ripoti ya upasuaji wa maiti ya mchuuzi wa barakoa aliyepigwa risasi kwa karibu na maafisa wa polisi wakati wa maandamano jijini Nairobi imebaini kuwa vipande 4 vya risasi vilibaki kwenye ubongo wa mchuuzi huyo Boniface Kariuki Mwangi.
Upasuaji wa maiti uliofanywa Alhamisi Julai 3, 2025 ulibaini kuwa Kariuki alifariki kutokana na majeraha ya kichwa yaliyosababishwa na risasi aliyopigwa na polisi siku hiyo.
Shughuli ya upasuaji huo iliendeshwa na wapasuaji wakiongozwa na daktari wa serikali Bernard Media kwa kushirikiana na daktari wa familia Peter Ndegwa.
Madaktari hao walibaini kuwa vipande vingine viwili viliondolewa na madaktari wakati Mwangi alipokuwa hai.
Uchunguzi huo haukuweza kuthibitisha kwa uhakika wakati halisi wa kifo chake huku madakrati wakieleza kuwa ubongo wa Mwangi huenda ulikuwa umekufa siku kadhaa kabla ya familia kuarifiwa rasmi.
Maafisa wa polisi wanaohusishwa na tukio hilo wanaendelea kuzuiliwa na polisi.
Mwangi alipigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya kushinikiza naibu inspekta wa polisi Eliud Lagat kujiuzulu, kufiatia kifo cha mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang’.
Baadaye Lagat alijiondoa ofisini kwa mda ili kupisha uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo, japo shinikizo za kuondoka ofisini kabisa ziliendelea kupitia maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z.
Mwanablogu huyo Ojwang’ atazikwa Julai 4, 2025 nyumbani kwao kaunti ya Homa bay.
Taarifa ya Joseph Jira.