Mchezaji kikosi cha Morans David Nyangige ni miongoni mwa wachezaji walioshtua wengi baada ya kujumuishwa katika kikosi cha Shujaa kilichotangazwa Jumatatu na kocha Kevin ‘Bling’ Wambua, wakati timu hiyo ikijiandaa kwa mashindano ya HSBC SVNS yatakayofanyika mwishoni mwa wiki hii katika Uwanja wa Nyayo.
Kikosi hicho cha wachezaji 12 kitaongozwa na nahodha George Ooro huku Samuel Asati akihudumu kama nahodha msaidizi. Wengine waliotajwa ni John Okoth, Dennis Abukuse, mkongwe Vincent Onyala, Kevin Wekesa, Patrick Odongo, Festus Shiasi, Nygel Amaitsa, Floyd Wabwire na Chrisant Ojwang.
Kocha Wambua alionyesha imani kubwa kwa kikosi chake akibainisha kuwa mashabiki wa nyumbani watatoa hamasa ya kipekee, hasa baada ya tiketi zote kuuzwa.
“Shinikizo tutakalopata tunalipokea kwa mikono miwili. Tukiwa nje ya nchi hupata nguvu kutoka kwa kona ya Wakenya, lakini wiki hii uwanja mzima ni kona ya Kenya. Tuna imani hilo litatupa msukumo mkubwa,” alisema Wambua.
Nahodha msaidizi Samuel Asati pia alieleza furaha yake kucheza nyumbani.
“Ni heshima kubwa kwangu kucheza nyumbani mwishoni mwa wiki hii. Tutafanya kila tuwezalo kuiletea nchi fahari tunapowania kufuzu kwa Divisheni ya Kwanza,” alisema Asati.
Kwa upande wa timu ya wanawake, Lionesses, kocha Simon Odongo amewajumuisha kwa mara ya kwanza Marvel Oswago na Charity Nilah. Wataungana na Naomi Amumgumi, Maureen Muritu, Sheila Chajira (Nahodha), Sinaida Nyacho, Edith Nariaka, Janet Okello, Freshia Oduor (Nahodha Msaidizi), Grace Okulu, Stella Wafula na Phoebe Akinyi.
Odongo alisifu uzoefu wa wachezaji wake wa kimataifa akisema unaongeza nguvu kikosini.
“Tunalenga kuipeperusha bendera ya Kenya juu wikendi hii mbele ya mashabiki wetu wa nyumbani,” alisema Odongo.
Katika mechi za ufunguzi, Shujaa watamenyana na Canada, Ubelgiji, Ujerumani, Uruguay na Marekani, huku Lionesses wakikabiliana na Brazil, China, Afrika Kusini, Argentina na Hispania.
Mashindano hayo yataanza Februari 14, yakifungua rasmi kampeni ya timu zote mbili ya kusaka nafasi ya kupanda Divisheni ya Kwanza. Kwa sasa Kenya ipo Divisheni ya Pili, lakini kumaliza miongoni mwa timu nne bora katika mfululizo wa mashindano ya raundi tatu kutawapa nafasi ya kupanda daraja, huku raundi ya kwanza ikifanyika nyumbani.
Wakati huo huo, mpango wa kukuza vipaji vya vijana wa Shirikisho la Raga Kenya umepata msukumo baada ya Kampuni ya Kenya Power (KPLC) kuahidi kutoa shilingi milioni 3 kusaidia programu za maendeleo ya raga mashinani. Wawakilishi wa KPLC walisisitiza umuhimu wa kulea vipaji vya vijana ili kuimarisha mustakabali wa raga nchini.
Hii hapa ni kikosi kamili cha Shujaa;
Shujaa:
George Ooro(Captain)
Samuel Asati (Co Captain)
John Okoth
Dennis Abukuse
Vincent Onyala
Kevin Wekesa
Patrick Odongo
Festus Shiasi
Nygel Amaitsa
Floyd Wabwire
Chrisant Ojwang
David Nyangige (Debut)
Lionesses
Naomi Amumgumi
Moreen Muritu
Sheila Chajira(Captain)
Sinaida Nyacho
Edith Nariaka
Janet Okello
Marvel Oswago (Debut)
Freshia Oduor (Co captain)
Charity Nilah (Debut)
Grace Okulu
Stella Wafula
Phoebe Akinyi
