News
Owen, awakosoa Wanaharakati wanaopinga kuapishwa kwa makamishna wa IEBC
Naibu kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Owen Baya amewashutumu baadhi ya wanaharakati walioelekea mahakamani kupinga kuapishwa kwa makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC akisema hatua hiyo inarudisha nyuma taifa la Kenya kimaendeleo.
Baya ambaye pia ni mbunge wa Kilifi Kaskazini kaunti ya Kilifi alisema hatua ya wanaharakati hao kupeleka kesi mahakamani inachelewesha kuapishwa kwa makamishna hao wa IEBC na hata kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo kwenye maeneo yanayokosa uwakilishi bungeni.
Baya alisema wakaazi wa eneo la Magarini kaunti ya Kilifi wamekuwa wakipitia changamoto nyingi kutokana na ukosefu wa uwakilishi bungeni.
Owen Baya pia alisema ikiwa wenyeji wa Magarini wataendelea kusalia bila Mbunge huenda wakakosa kutekelezewa miradi ya maendeleo licha ya kuwa ni haki yao kikatiba.
“Wale ambao wako na haraka ya kuenda mahakamani, kuzuia maneno ya kuapishwa kwa watu wa IEBC wanafanyia watu wa Magarini mambo mabaya sana.Wamekaa bila uongozi kwa muda mrefu’’ alisema Owen
Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa Magarini Harry Kombe alitaka wanaharakati waliolekea mahakamani kupinga kuapishwa kwa makamishna wa tume ya IEBC kuondoa kesi hiyo mahakamani ili wananchi wapewe fursa ya kushiriki uchaguzi.
Taarifa ya Janet Mumbi