Vocal Africa yamtaka Wetangula na Kingi kujiuzulu

Vocal Africa yamtaka Wetangula na Kingi kujiuzulu

Shinikizo linaendelea kumkabili Spika wa bunge la kitaifa, Moses Wetang’ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi baada ya maombi mapya ya kumtia hatiani kwa kudharau amri ya Mahakama kuwasilishwa Mahakamani.

Maombi hayo, yaliowasilishwa na Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Vocal Africa, yanawashutumu viongozi hao wawili kwa kukaidi amri ya Mahakama inayowazuia kushiriki katika siasa za vyama.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa mbele ya Jaji wa Mahakama kuu ya Milimani David Mburu, aliidhinisha maombi hayo kama ya dharura na akaagiza yahudumiwe mara moja.

Shirika la Vocal Africa chini ya Mkurugenzi wake Hussein Khalid wamemtaka Spika Wetang’ula na Kingi, kujiuzulu na kuingia kwenye ulingo wa siasa iwapo hawatazingatia amri ya Mahakama.

“Tunashangaa kwa nini viongozi hawa wawili Spika Wetangula na Kingi kujiusisha na siasa kwa kutumia ushawishi wao na raslimali za umma kumpigia debe rais Ruto wakati wako na jukumu la kikatiba kusimamia shughuli za kiserikali, ndio tunasema heri wajiuzulu kisha waingie siasa”, alisema Khalid.

Mahakama hiyo hata hivyo inatarajiwa kutoa maelekezo zaidi kuhusu kesi hiyo mnamo tarehe 16 mwezi Julai mwaka huu.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi