Mahakama ya Kilifi yamuachilia huru mshukiwa wa kesi ya unajisi

Mahakama ya Kilifi yamuachilia huru mshukiwa wa kesi ya unajisi

Mahakama ya Kilifi imemuachilia huru mwanaume mmoja aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya unajisi.

John Mwatule Daniel aliachiliwa huru baada ya kesi iliyowasilishwa Mahakamani dhidi yake kukosa ushahidi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kwamba mshukiwa alihusika katika kuteleleza kitendo hicho.

Mahakama pia ilibaini kwamba mashihidi waliowasilishwa Mahakamani na upande wa mashtaka, ushahidi wao ulikinzana na kesi hiyo.

John alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la kumjansi mtoto wake wa kambo mnamo mwezi Julai mwaka 2022 na kudaiwa kwamba alimtishia na kisu endapo angekataa kufanya kitendo hicho.

Hata hivyo, wakati wa kujitetea mtuhumiwa alieleza Mahakama kwamba kulikuwepo na uhasama baina yake na upande wa familia ya mtoto huyo ambaye alikuwa binti yake wa kambo.

“Tumekuwa na shida kidogo na familia ya mtoto huyo na ndiposa wakanisingizia lakini mimi sijafanya kosa lolote kwa mtoto huyo kwa sasa ni binti yangu”, aliambia Mahakama mshukiwa.

Hakimu wa Mahakama hiyo James Mwaniki alisema Mahakama ilizingatia ushahidi wa pande zote mbili na kwamba Mahakama ikabaini kwamba mtuhumiwa hana hatia na akaachiliwa huru.

“Mahakama imesikiza pande zote mbili wakati wa kesi hii ilipoletwa hapa Mahakama na tumebaini kwamba ushahidi uliyowasilishwa Mahakama dhidi ya mshukiwa haukuwa na uzito wa kuilazimisha Mahakama kumpata na hatia. Kwa hivyo Mahakama imechukua hatua ya kumuachilia huru mshukiwa”, alitoa amri hiyo Hakimu.

Taarifa ya Teclar Yeri