Idara ya usalama kanda ya Pwani imewaonya wananchi wanaomiliki silaha haramu katika kaunti ya Tana river.
Mshirikishi wa utawala kanda ya Pwani Paul Rotich aliwataka wanaomiliki silaha hizo kuzisalimisha mara moja kwa maafisa wa polisi katika kituoc cha polisi kiilichokaribu nao.
Akizungumza katika kikao cha kiusalama kaunti ya Tana river, Rotich alisema oparesheni ya kusaka silaha hizo imeenzishwa huku akiwaagiza machifu na manaibu wao kushirikiana na maafisa wa polisi ili kuhakikisha silaha hizo zinapatikana.
Rotich alisema zaidi ya bunduki 120 ziko mikononi mwa raia wa maeneo ya Bangale na Tana Kaskazini katika kaunti ya Tana river, akisema ni lazima zirudishwe kwa serikali.
“Tunataka zile bunduki zote mnazomiliki kinyume cha sheria mrudishe kwanza ndio tuongee mambo ingine, haiwezekana mnamiliki bunduki haramu na mnataka serikali iwalinde kwani mtaishi na majangili mpaka lini, hiyo maneno hatutakubali rudisheni bunduki ama tutaanzisha oparesheni kali”, alisema Rotich.
Hata hivyo wakaazi wa kaunti hiyo wamepongeza hatua hiyo ya serikali, wakiwarai wenyeji kukumbatia amani ili kuepuka umwagikaji wa damu katika kaunti hiyo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
